Na Christopher Nyenyembe, Mbeya.
|
Christopher Nyenyembe (TanzaniaDaima Mbeya) |
HIVI leo, Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) anapotamka hadharani kuwa CCM waache kutegemea
polisi ana maanisha nini?
Sijui anataka kuwaambia nini Watanzania wa leo kuwa jitihada kubwa za
kukijenga chama hicho na nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola
wakati wa uchaguzi mkuu, rais alikuwa haoni.
Sijui anatoa darasa gani kwa wana CCM wenzake kuwa waache tabia ya
kuwategemea polisi katika harakati zao za kisiasa akisahau kuwa polisi
ndio wanaotumika kuwasambaratisha wafuasi wa vyama vingine vya siasa
vinapotekeleza majukumu yao ya kisiasa.
Kauli ya Rais Kikwete kama ilivyonukuliwa na vyombo vya habari mjini
Dodoma wiki hii alipokuwa akifunga mkutano mkuu wa nane wa CCM, moja ya
kauli yake ilikuwa kukionya chama anachokiongoza kuwa kisiwategemee
polisi katika masuala ya kisiasa, kwa kuwa kufanya hivyo CCM watakuwa
wakijidanganya.
Onyo hilo la rais kama mwenyekiti wa chama cha siasa anachokiongoza
linatia shaka kwa kuwa naamini zuio hilo limetolewa muda ambao yeye
binafsi anajua fika kuwa hagombei tena urais mwaka 2015.
Alikuwa wapi kuwazuia polisi waliowapiga mabomu wananchi wa mkoa wa
Arusha wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, waliopigwa mabomu
Mwanza, Mbeya, Morogoro, Singida na Dar es Salaam ili watu waogope
kwenda kupiga kura.
Siamini na sidhani kama agizo la mwenyekiti wa chama hicho, ambaye ni
kiongozi mkuu wa chama hicho kikongwe cha siasa kuwa ndiyo dhamira ya
kweli ya kukitaka chama hicho kiache kutegemea polisi katika masuala yao
ya kisiasa.
Sitaki kujirudisha kwenye maumivu makali ya kisiasa na namna polisi
walivyoweza kutumika kuvuruga shughuli za kisiasa zinazoendelea kufanywa
na vyama vya upinzani, hususan CHADEMA siku waliyofurumshwa na mabomu
kule Nyololo, Mufindi, Mkoa wa Iringa.
Polisi hao walifanya kazi ya kutuliza vurugu ambazo hazikuwepo na
hatimaye kusababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel
Ten, marehemu Daudi Mwangosi, katika tukio hilo niliamini fika kuwa
katika kukemea nguvu kubwa inayotumiwa na polisi katika masuala ya
kisiasa, Rais Kikwete angetoa pole kwa familia ya marehemu lakini
hakufanya hivyo.
Nilisema na narudia kusema tena kuwa situmi ombi kwa rais kutaka
kumwambia kuwa, watoto wa marehemu Mwangosi wanamlilia, na hata Mwangosi
mwenyewe anamlilia anauliza Rais Kikwete uko wapi Mwangosi ninakulilia?
Hayo yamepita, leo hii Mwenyekiti wa CCM anakionya chama chake eti
kisitegemee polisi.
Kwa maana hiyo na matukio kadhaa yanayotokea dhidi ya vyama vya
upinzani ambapo polisi walioajiriwa na serikali inayoongozwa na CCM kuwa
ni kweli wanatumwa na chama hicho ili kuvidhibiti vyama vingine vya
siasa vinavyotishia uhai wa CCM.
Iweje kama nguvu kubwa zimekuwa zikitumika kuvizima vyama pinzani ili
kudhoofisha harakati zao za kujijenga, leo hii itawezekana vipi kama
rais huyo huyo akiwa Mwenyekiti wa CCM taifa ameirudisha safu mpya
iliyokuwa chini ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na
kuwataka viongozi hao wasitegemee polisi.
Yapo maswali ya kujiuliza kuwa enzi za kina Philip Mangula,
Abdulrahaman Kinana, Seif Khatib na Mama Zakhia Meghji wakiwa kwenye
safu ya Mkapa walikuwa hawategemei polisi ili kuendesha harakati zao za
kisiasa na kama walikuwa wanategemea polisi wamerudishwa upya ili waache
kutegemea polisi ?
Nauliza nikiamini kuwa uzoefu wa CCM wa kutegemea polisi katika
masuala yake ya kisiasa ulianza lini, ulianza kabla ya mfumo wa vyama
vingi vya siasa au ulianza baada ya kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi
ndipo CCM walipogundua kuwa polisi ni mali yao.
Na kama miaka yote CCM wanaamini kuwa polisi ni mali ya CCM na vyama
vingine vya siasa havina polisi, kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama
hicho aliyoitoa mkoani Dodoma ya kukionya chama chake kisitegemee polisi
anataka kuwaambia nini Watanzania ambao bado wapo usingizini.
Lakini ni vema ninukuu kwa undani kile alichokisema juu ya CCM na
utegemezi wa nguvu za polisi, kuwa kitendo cha wana CCM kuishi katika
siasa kwa kutegemea Jeshi la polisi hakipaswi kukubaliwa kwa kuwa
kimepitwa na wakati.
“Mnaishia kulalamika tu kila siku eti wanatukana halafu mnaishia
kusema kawaida yao… au utasikia mtu anasema eti serikali haipo!Kazi ya
serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu,”
alisema Kikwete alipokuwa akifunga mkutano huo.
“Sasa mnataka wakisema serikali ya CCM haijafanya kitu,polisi
wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wawakamate ? Kama
wakisema hatujafanya kitu, ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu,
waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.
“Mkijibu kwa hoja wanatulia, siyo polisi. Nakumbuka Mwigulu aliwajibu
pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu akasimama
na kupigilia msumari kweli wakachanganyikiwa sasa hizo ndio kazi
zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.
Kama, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete ameamua kukiambia chama
chake leo kuwa kisitegemee polisi, alikuwa wapi kukionya mara tu
alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kutoa kauli hiyo katika mkutano mkuu wa
saba alipochukua mikoba iliyoachwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Nini kimetokea ndani ya CCM na safu yake mpya inayoelekea kwenye
vuguvugu la uchaguzi wa mwaka 2015 huku kukiwa na zuio kubwa la kukitaka
chama hicho kiendeshe masuala yake ya kisiasa bila kutegemea polisi,
wameona hasara gani ya kutumia polisi.
Naamini kuwa mtaji mkubwa wa CCM katika medani ya kisiasa imekuwa
ikielekezwa kwenye matumizi ya nguvu za vyombo vya dola siyo polisi
pekee yao ambao CCM wanatakiwa waache kuvitumia, waache kabisa kutumia
raslimali za nchi kwa lengo la kukijenga chama chao, waache ili serikali
iwe salama.
Kama CCM wanaambiwa hivyo leo, basi Rais Kikwete hakuona alipokuwa
akihutubia mkutano huo jinsi watendaji wa serikali walivyokuwa
wamejazana Dodoma wakiwa ndani ya ukumbi wa Kizota, huku ni wakuu wa
wilaya na mikoa na upande wa pili ni wajumbe wa kamati za siasa za chama
hicho.
Watendaji wengi wa serikali wametumia kwa kiasi kikubwa raslimali za
nchi na kulipwa masurufu kwa kazi za chama, mara baada ya mkutano huo
kumalizika wamebaki Dodoma kwa kigezo cha kushiriki kwenye mrejesho wa
semina elekezi kwa watendaji wa serikali hayo ndio maajabu ya CCM.
Rais Kikwete anapaswa kusoma alama za nyakati kuwa Watanzania wa leo
hawaamini moja kwa moja mawazo ya mtu mmoja ili kuweza kuijenga nchi
yenye utawala bora bila kukiuka misingi madhubuti ya haki za binadamu.
Kwa kuwa haki za binadamu zimekuwa zikikiukwa kwa misingi pengine ya
kukibeba chama tawala ili kiendelee kushika dola hata kama wananchi
wamechoka, rais alipaswa kuliagiza Jeshi la Polisi kuwa liache kuingilia
masuala ya kisiasa na si kukiambia chama chake kuwa kisitegemee polisi,
hilo si zuio ni agizo la kiutendaji kwa upande wa pili wa shilingi.
Naamini kuwa ili nchi iweze kujielekeza kwenye ujenzi wa demokrasia ya
kweli ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, basi kila chama
kinapaswa kuheshimu sheria za nchi na taratibu zote za kuendesha vyama
vya siasa ili kuepuka vurugu.
Jeshi la Polisi nao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria ili chombo
hicho kisitafsiriwe kuwa ni mali ya CCM na ili kuondoa dhana hiyo
polisi wamesikia, kuwa CCM sasa haitawategemea tena.