Nov 18, 2012

C. NYENYEMBE: CCM WANATEGEMEA POLISI?

Na Christopher Nyenyembe, Mbeya.
Christopher Nyenyembe (TanzaniaDaima Mbeya)
HIVI leo, Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anapotamka hadharani kuwa CCM waache kutegemea polisi ana maanisha nini?

Sijui anataka kuwaambia nini Watanzania wa leo kuwa jitihada kubwa za kukijenga chama hicho na nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola wakati wa uchaguzi mkuu, rais alikuwa haoni.

Sijui anatoa darasa gani kwa wana CCM wenzake kuwa waache tabia ya kuwategemea polisi katika harakati zao za kisiasa akisahau kuwa polisi ndio wanaotumika kuwasambaratisha wafuasi wa vyama vingine vya siasa vinapotekeleza majukumu yao ya kisiasa.

Kauli ya Rais Kikwete kama ilivyonukuliwa na vyombo vya habari mjini Dodoma wiki hii alipokuwa akifunga mkutano mkuu wa nane wa CCM, moja ya kauli yake ilikuwa kukionya chama anachokiongoza kuwa kisiwategemee polisi katika masuala ya kisiasa, kwa kuwa kufanya hivyo CCM watakuwa wakijidanganya.

Onyo hilo la rais kama mwenyekiti wa chama cha siasa anachokiongoza linatia shaka kwa kuwa naamini zuio hilo limetolewa muda ambao yeye binafsi anajua fika kuwa hagombei tena urais mwaka 2015.

Alikuwa wapi kuwazuia polisi waliowapiga mabomu wananchi wa mkoa wa Arusha wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, waliopigwa mabomu Mwanza, Mbeya, Morogoro, Singida na Dar es Salaam ili watu waogope kwenda kupiga kura.

Siamini na sidhani kama agizo la mwenyekiti wa chama hicho, ambaye ni kiongozi mkuu wa chama hicho kikongwe cha siasa kuwa ndiyo dhamira ya kweli ya kukitaka chama hicho kiache kutegemea polisi katika masuala yao ya kisiasa.

Sitaki kujirudisha kwenye maumivu makali ya kisiasa na namna polisi walivyoweza kutumika kuvuruga shughuli za kisiasa zinazoendelea kufanywa na vyama vya upinzani, hususan CHADEMA siku waliyofurumshwa na mabomu kule Nyololo, Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Polisi hao walifanya kazi ya kutuliza vurugu ambazo hazikuwepo na hatimaye kusababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, katika tukio hilo niliamini fika kuwa katika kukemea nguvu kubwa inayotumiwa na polisi katika masuala ya kisiasa, Rais Kikwete angetoa pole kwa familia ya marehemu lakini hakufanya hivyo.

Nilisema na narudia kusema tena kuwa situmi ombi kwa rais kutaka kumwambia kuwa, watoto wa marehemu Mwangosi wanamlilia, na hata Mwangosi mwenyewe anamlilia anauliza Rais Kikwete uko wapi Mwangosi ninakulilia? Hayo yamepita, leo hii Mwenyekiti wa CCM anakionya chama chake eti kisitegemee polisi.

Kwa maana hiyo na matukio kadhaa yanayotokea dhidi ya vyama vya upinzani ambapo polisi walioajiriwa na serikali inayoongozwa na CCM kuwa ni kweli wanatumwa na chama hicho ili kuvidhibiti vyama vingine vya siasa vinavyotishia uhai wa CCM.

Iweje kama nguvu kubwa zimekuwa zikitumika kuvizima vyama pinzani ili kudhoofisha harakati zao za kujijenga, leo hii itawezekana vipi kama rais huyo huyo akiwa Mwenyekiti wa CCM taifa ameirudisha safu mpya iliyokuwa chini ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na kuwataka viongozi hao wasitegemee polisi.

Yapo maswali ya kujiuliza kuwa enzi za kina Philip Mangula, Abdulrahaman Kinana, Seif Khatib na Mama Zakhia Meghji wakiwa kwenye safu ya Mkapa walikuwa hawategemei polisi ili kuendesha harakati zao za kisiasa na kama walikuwa wanategemea polisi wamerudishwa upya ili waache kutegemea polisi ?

Nauliza nikiamini kuwa uzoefu wa CCM wa kutegemea polisi katika masuala yake ya kisiasa ulianza lini, ulianza kabla ya mfumo wa vyama vingi vya siasa au ulianza baada ya kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi ndipo CCM walipogundua kuwa polisi ni mali yao.

Na kama miaka yote CCM wanaamini kuwa polisi ni mali ya CCM na vyama vingine vya siasa havina polisi, kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho aliyoitoa mkoani Dodoma ya kukionya chama chake kisitegemee polisi anataka kuwaambia nini Watanzania ambao bado wapo usingizini.

Lakini ni vema ninukuu kwa undani kile alichokisema juu ya CCM na utegemezi wa nguvu za polisi, kuwa kitendo cha wana CCM kuishi katika siasa kwa kutegemea Jeshi la polisi hakipaswi kukubaliwa kwa kuwa kimepitwa na wakati.

“Mnaishia kulalamika tu kila siku eti wanatukana halafu mnaishia kusema kawaida yao… au utasikia mtu anasema eti serikali haipo!Kazi ya serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu,” alisema Kikwete alipokuwa akifunga mkutano huo.

“Sasa mnataka wakisema serikali ya CCM haijafanya kitu,polisi wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wawakamate ? Kama wakisema hatujafanya kitu, ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.

“Mkijibu kwa hoja wanatulia, siyo polisi. Nakumbuka Mwigulu aliwajibu pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu akasimama na kupigilia msumari kweli wakachanganyikiwa sasa hizo ndio kazi zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.

Kama, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete ameamua kukiambia chama chake leo kuwa kisitegemee polisi, alikuwa wapi kukionya mara tu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kutoa kauli hiyo katika mkutano mkuu wa saba alipochukua mikoba iliyoachwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Nini kimetokea ndani ya CCM na safu yake mpya inayoelekea kwenye vuguvugu la uchaguzi wa mwaka 2015 huku kukiwa na zuio kubwa la kukitaka chama hicho kiendeshe masuala yake ya kisiasa bila kutegemea polisi, wameona hasara gani ya kutumia polisi.

Naamini kuwa mtaji mkubwa wa CCM katika medani ya kisiasa imekuwa ikielekezwa kwenye matumizi ya nguvu za vyombo vya dola siyo polisi pekee yao ambao CCM wanatakiwa waache kuvitumia, waache kabisa kutumia raslimali za nchi kwa lengo la kukijenga chama chao, waache ili serikali iwe salama.

Kama CCM wanaambiwa hivyo leo, basi Rais Kikwete hakuona alipokuwa akihutubia mkutano huo jinsi watendaji wa serikali walivyokuwa wamejazana Dodoma wakiwa ndani ya ukumbi wa Kizota, huku ni wakuu wa wilaya na mikoa na upande wa pili ni wajumbe wa kamati za siasa za chama hicho.

Watendaji wengi wa serikali wametumia kwa kiasi kikubwa raslimali za nchi na kulipwa masurufu kwa kazi za chama, mara baada ya mkutano huo kumalizika wamebaki Dodoma kwa kigezo cha kushiriki kwenye mrejesho wa semina elekezi kwa watendaji wa serikali hayo ndio maajabu ya CCM.

Rais Kikwete anapaswa kusoma alama za nyakati kuwa Watanzania wa leo hawaamini moja kwa moja mawazo ya mtu mmoja ili kuweza kuijenga nchi yenye utawala bora bila kukiuka misingi madhubuti ya haki za binadamu.

Kwa kuwa haki za binadamu zimekuwa zikikiukwa kwa misingi pengine ya kukibeba chama tawala ili kiendelee kushika dola hata kama wananchi wamechoka, rais alipaswa kuliagiza Jeshi la Polisi kuwa liache kuingilia masuala ya kisiasa na si kukiambia chama chake kuwa kisitegemee polisi, hilo si zuio ni agizo la kiutendaji kwa upande wa pili wa shilingi.

Naamini kuwa ili nchi iweze kujielekeza kwenye ujenzi wa demokrasia ya kweli ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, basi kila chama kinapaswa kuheshimu sheria za nchi na taratibu zote za kuendesha vyama vya siasa ili kuepuka vurugu.

Jeshi la Polisi nao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria ili chombo hicho kisitafsiriwe kuwa ni mali ya CCM na ili kuondoa dhana hiyo polisi wamesikia, kuwa CCM sasa haitawategemea tena.