Mchezaji wa kati wa timu ya soka ya Manchester City ya Uingereza, Yaya
Toure, amenyakua tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka la
Afrika, CAF.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amenyakua tuzo
hiyo na kuwapiku washindani wake wawili Didier Drogba anayesakata
kabumbu katika timu ya soka ya Galatasaray ya Uturuki na kiungo wa
Chelsea na timu ya taifa ya Nigeria John Obi Mikel.
Hii ni mara ya tatu
mfululizo kwa Yaya Toure kushinda tuzo ya mchezaji bora wa CAF, baada ya
mwaka 2011 na 2012 kujinyakulia pia tuzo hiyo. Wakati huo huo kocha wa
timu ya soka ya taifa ya Nigeria Stephen Keshi amenyakua tuzo ya kocha
bora wa mwaka barani Afrika katika soka.
Katika sherehe za kuwatangaza
waliong'ara katika soka barani Afrika mwaka 2013 huko Lagos Nigeria,
Keshi alishinda tuzo ya kocha bora.