Jan 7, 2014

Historia: Siku kama ya leo miaka 690 Iliyopita

Siku kama ya leo miaka 690 alifariki dunia mtalii mashuhuri wa Kiitalia Marco Polo. Alizaliwa katika mji wa Venice nchini Italia na alianza safari iliyokuwa na mikasa mingi akiwa na umri wa miaka 18 akiwa pamoja na baba yake. Safari ya kitalii ya Polo katika nchi za Mashariki iliendelea kwa kipindi cha miaka 20.
Alirejea nchini Italia mwaka 1291 na kuandika aliyoyaona katika kitabu alichokipa jina la "Maajabu". Kitabu hicho kilipata umashuhuri mkubwa duniani na alizungumzia kwa mapana na marefu kuhusu aliyoyaona katika nchi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia.
Siku kama ya leo miaka 372 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78.
Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari

Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Mwislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani miaka 7 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran. Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran".