WATU kadhaa wanahofiwa kupoteza maisha ikiwa 5 wathibitishwa kufa baada ya boti ya MV Kilimanjaro 2 inayomilikwa na shirika la Azam Marine kukumbwa na dhoruba katikati ya bahari, wakati ilipokuwa safarini kutoka kisiwani Pemba kuelekea kisiwani Unguja.
Baadhi ya habari nchini Tanzania zimelinukuu jeshi la polisi likidai kuwa, baadhi ya abiria waliokuwemo kwenye boti hiyo walichukua majaketi ya kujiokolea na kuyatupa nje ya boti hiyo.
Hata hivyo watu mbalimbali waliokuwemo kwenye boti hiyo walipohojiwa na vyombo vya habari wamesema kuwa majaketi yaliyokuwemo yalikuwa hayatoshi na watu waliyapata kwa kugombania.
Hadi hivi sasa idadi hasa ya watu waliopoteza maisha yao haijajulikana. Taarifa zinaongeza kuwa, boti hiyo ilikuwa na abiria 69 watu wazima, abiria watoto 60 na mabaharia wanane.
Iliondoka saa mbili asubuhi kisiwani Pemba kuelekea kisiwani Unguja, na ilipofika katika eneo la Nungwi bahari ilichafuka na boti ikaanza kuyumba.