Jan 2, 2014

LEO katika Historia, Miaka 1435 iliyopita...


Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita, Mtume Muhammad SAW alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihajiri Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah tayari ameshaondoka mjini Makka. Inafaa kuashiria hapa kuwa, tukio la kuhajiri Mtume SAW lilikuwa ni mwanzo wa kalenda ya Kiislamu, kwani barua zote zilizokuwa zikipelekwa kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu zilikuwa zikiandikwa kwa kufuata kalenda hiyo.Siku kama ya leo miaka 1370 inayosadifiana na tarehe Mosi Rabiul Awwal mwaka 65 Hijria, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Suleiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Januri 1993, yalitiwa saini  makubaliano ya kupunguza silaha za atomiki kati ya Boris Yeltsin, Rais wa zamani wa Russia na George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zilipaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za atomiki. Hata hivyo, mnamo mwezi Aprili mwaka 2010 Russsia na Marekani zilitiliana saini makubaliano mapya ya START ambayo yalikuwa na lengo la kupunguza vichwa vya makombora 1,550 ya nyuklia.
Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alimtumia ujumbe Mikhail Gorbachev, Rais wa mwisho wa Urusi ya zamani akimtaka  asilimu na kuachana na fikra za Kimaksi. Ujumbe huo wa Imam Khomeini MA ulipelekwa na Ayatullah Jawad Amoli, mmoja wa maulama wakubwa hapa nchini.