Jan 26, 2014

Leo katika Historia, Miaka 114 iliyopita, kutoka Iran

Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita mfamasia wa Kijerumani Felix Hoffmann alitengeneza dawa ya kwanza ya kutuliza maumivu. Dawa hiyo hii leo inajulikana kwa jina la Aspirin. Waingereza pia waliamua kutengeneza dawa hiyo katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya uingizaji dawa hiyo nchini Uingereza kusimamishwa. Mbali na kutuliza maumivu, Aspirin ina sifa nyingine kadhaa ambazo ni pamoja na kuzuia damu isigande na kuzuia mshtuko wa moyo.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini vilisitishwa, lakini kwa hakika serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964.
Na miaka 35 iliyopita katika siku kama leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiunga mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho.
Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano.