Chama cha walimu (CWT) kimesema
pamoja na bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Mahakama kuagiza
chama hicho na serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la
kuyapatia ufumbuzi madai ya walimu, bado serikali haijaonyesha utayari
wowote wa kufanya hivyo.
Rais wa CWT Gratian Mukoba
amesema chama kimechukua hatua mbalimbali ikiwemo kumwandikia barua
katibu mkuu kiongozi zaidi ya mara moja kuonyesha utayari wa CWT
kukutana na Serikali kwa majadiliano lakini hadi sasa hakuna taarifa
yoyote kutoka serikalini.
Amesema kitendo cha serikali
kukaa kimya kwa muda wa siku 27 bila kuonyesha kujali kutekelezwa kwa
amri ya Mahakama, kinatafsiriwa na CWT kama ni kukosekana kwa nia njema
ya serikali kusikiliza madai ya walimu.
Kwenye line nyingine, CWT
kimeitaka serikali kuwaachia huru baadhi ya viongozi wa CWT na walimu
wote waliofunguliwa mashtaka ikiwa ni pamoja na kuwarejeshea madaraka
walimu 15 waliovuliwa vyeo vyao kutokana na mgomo wa walimu.