Mzee Nelson
Mandela aliyefariki dunia usiku wa 05/12/2013, alizaliwa mwaka 1918 na
hatimaye kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini baada ya kuongoza
mapambano ya muda mrefu dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu.
Mandela ambaye nchini Afrika
Kusini anajulikana kwa jina la MADIBA, alifungwa jela kwa kipindi cha miaka 27
katika kisiwa cha Robben kutokana na harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi
na kupigania uhuru wa nchi ya Afrika Kusini.
Baada ya kuachiwa kwake huru Februari 11
mwaka 1990 alihamasisha siasa za amani na suluhu, suala ambalo lilirahisisha
mchakato wa kuiondoa Afrika Kusini katika utawala wa wazungu wachache na
kuelekea kwenye demokrasia.
Katika kipindi chote cha miongo minne ya
harakati zake za kisiasa Mzee Mandela ametunukiwa zaidi na tuzo 250 ikiwemo
tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1993.
PAMOJA
NA HAYO.
Kutokana na mapambano yake dhidi ya ubaguzi
wa rangi na kupigania uhuru wa Afrika Kusini nchi za Magharibi zilizokuwa
zikiwaunga mkono makaburu wabaguzi zilimtambua Mandela kuwa ni gaidi.
Shujaa huyo wa Afrika aliwekwa kwenye orodha
ya magaidi ya Marekani kwa miaka mingi na aliendelea kuwekwa kwenye orodha ya
magaidi ya serikali ya Washington hata wakati alipokuwa Rais aliyechaguliwa na
wananchi.
Mandela aliondolewa kwenye orodha ya magaidi
ya Marekani mwaka 2008. Kuwekwa jina la mpigania uhuru mkubwa wa Afrika katika
orodha ya magaidi ya Marekani kunafichua na kuweka wazi maana ya ugaidi katika
kamusi ya kisiasa ya nchi hizo za Magharibi.