KATIKA maadhimisho ya siku ya Ukimwi, Wakazi wa jijini na mkoa wa Mbeya wamelalamikia vitendo vya waathirika wa Ukimwi kusambaza ugonjwa huo kwa makusudi kwa dhana iliyojengeka kuwa ‘’Tufe wengi’’.
Wakiongea na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe kulikofanyika maaadhimisho hayo kimkoa walilalamikia suala hilo kwa huzuni huku wakiwasihi wenye tabia hizo kuacha mara moja.
‘’Kweli unaweza kuishi muda mrefu na maambukizo ya Ukimwi lakini sio iwe sababu kusambaza hata kama unaogopa watu wajue kuwa umeathirika basi tutumie zana (kondom)’’ alisema mkazi mmoja.
Bi Helena Julius, yeye amejiunga na shirika la (SHIDEFA) linalojihusisha na kutoa elimu kwa waathirika wa Ukimwi ambapo yeye anaishi na maambukizo ya Ukimwi tangu Agosti mwaka 2005.
Nao wamelizungumzia suala hilo na kuwa hiyo imekuwa ni moja kati ya changamoto kwao na kwamba wanajitahidi kadri ya uwezo wao ingawa bado kunakuwa na watu wasiokuwa waelewa.
‘’Nawasihi watu wawe waelea juu ya janga hili na waone kama kulitokomeza inawezekana’’ alisema Helen Julius.