SHILINGI Milioni Moja na laki tatu zimetolewa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) katika shule ya sekondari ya Itamba iliyopo wilaya ya Ileje mkoani Mbeya ili kutatua kero ya maji iliyopo shuleni hapo.
Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne shuleni hapo mwakilishi wa Kampuni hiyo Nyanda za Juu Kusini, Herbert Irembo, alisema katika jamii hususani ya wanafunzi inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo shule nyingi kuanzishwa bila huduma za msingi kama maji.
“Hivyo tumeliona hilo na kuamua kutoa kiasi hicho cha pesa ili kuwasaidia wanafunzi na walimu wa shule hii kufanya kazi katika mazingira mazuri kama mjuavyo maji ni uhai yasipokuwepo ni matatizo” alisema Irembo.
Akipokea msaada huo na kuishukuru kampuni hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Peter Siame, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2007, kumekuwa na kero ya maji hivyo kuwapa tabu walimu na wanafunzi katika utendaji wa kazi kutokana na kuyafuata umbali mrefu.
Pia mkuu huyowa shule alisema kuwa kero hiyo imekuwa sababu ya wanafunzi kuwa watoro wakati wanapotumwa kuchota maji katika umbali huo mrefu.
Aidha, Irembo aliwaasa wahitimu wa kidato cha nne kuwa wavumilivu pindi watakapokuwa wakisubiri matokea yao ya kwani imeonekana vijana wengi wanapohitimu masomo yao hujiingiza katika vitendo viovu kutokana na tamaa ya pesa.